Jumapili, 19 Julai 2015

TABIA YA MBINGUNI HAINA BUDI KUPATIKANA DUNIANI:

Msidanganyike. Mungu hadhihakiwi. Utakatifu tu, wala si kitu kingine, ndio utakaowafanya kuwa tayari kwenda mbinguni. Unyofu na uchaji wa hakika ktk mambo ya maisha peke yake ndio uwezo wa kuwapa tabia safi, na bora, na kuwawezesha kuingia mbele za Mungu akaaye penye nuru isiyoweza kukaribiwa. Tabia ya mbinguni haina budi kupatikana hapa duniani, ama sivyo kamwe haipatikani tena. Basi, anza mara moja. Usidanganyike kuwa utafika wakati uwezapo kujitahidi kwa urahisi kuliko sasa. Kila siku huzidisha umbali wako kutoka kwa Mungu. Jitayarishe kwa ajili ya uzima wa milele. Zoeza mawazo ya moyo wako kuipenda Biblia, kupenda mikutano ya maombi, kupenda saa ya kumtafakari Mungu, na, zaidi ya yote, saa ambayo roho hushirikiana na Mungu. Uwe mwenye kufikiri mambo ya mbinguni ukipenda kuungana, na lile kundi la waimbaji wa mbinguni ktk makao ya juu.

Jumanne, 14 Julai 2015

MASOMO YANAYOHARIBU ROHO YA MTU: (PART 3)

Chimbuko lingine la hatari ambalo twapaswa kujihadhari nalo siku zote ni kusoma vitabu vilivyotungwa na makafiri. Vitabu vya namna hiyo huandikwa kwa uongozi wa yule adui wa ukweli, na hakuna mtu awaye yote awezaye kuvisoma bila kuihatarisha roho. Kwa kweli wengine wanaoathirika na vitabu hivyo hatimaye huweza kupona; wote wanaojituliza kwa mvuto mbaya wa vitabu hivyo hujiweka ktk milki ya Shetani, naye huwafaidi sana. Wakiyakaribisha majaribu yake jinsi hiyo, hawana hekima ya kupambanua wala nguvu za kuyapinga. Kwa uwezo wa mivuto ya uzuri unaopoteza akili, kutoamini na ukafiri huimarika akilini.

MASOMO YANAYOHARIBU ROHO YA MTU: (PART 2)

Katika mafundisho ya watoto na vijana, hekaya, hadithi za kizimwi, na hadithi za uongo sasa zimepewa nafasi kubwa. Vitabu vya namna hiyo hutumika shuleni, navyo hupatikana nyumbani mwa watu wengi. Wazazi ambao ni Wakristo huwezaje kuwaruhusu watoto wao kutumia vitabu vilivyojaa uongo jinsi hii? Watoto wakiuliza maana ya hadithi hizo ambazo ni kinyume cha mafundisho ya wazazi wao, hujibiwa kuwa hadithi hizo si za kweli; lakini hili halisaidii kuwaepusha na matokeo mabaya ya kuzitumia. Mawazo yatolewayo ktk vitabu hivyo huwapotosha watoto. Huingiza maoni ya uongo ya maisha na kuzaa pamoja na kuchochea tamaa ya mambo yasiyo ya hakika, yakuwaziwa tu. Kamwe vitabu vyenye kuipotosha kweli visiwekwe mikononi mwa watoto au vijana. Watoto wetu wanapojielimisha kwa njia hii, wasiruhusiwe kuwa na mawazo ambayo yatakuwa mbegu za dhambi.

MASOMO YANAYOHARIBU ROHO YA MTU:

Kwa ajili ya wingi wa vitabu na magazeti vinavyomiminika daima kutoka ktk mitambo ya kuchapisha, wazee kwa vijana hufanya mazoea ya kusoma haraka-haraka na kwa juu juu tu, na hivyo ubongo hupoteza uwezo wake wa kupokea mawazo yaliyounganika na yenye nguvu. Juu ya hayo, sehemu kubwa ya magazeti na vitabu ambavyo, kama vyura wa Misri, vinatapakaa nchini, sio kwamba nivya hali ya chini tu, visivyofaa, na vyenye kudhoofisha, bali ni vichafu na vyenye kuaibisha. Matokeo yake siyo kulevya na kuharibu akili tu, bali kuchafua na kuangamiza roho.